Kuvunjwa kwa meza na vibanda vya akina mama wanaofanya biashara ndogondogo katika maeneo ya wakazi wa kipato cha chini.
Submitted by Mwananchi on Thu, 2006-10-12 17:29.
Uchumi
Jina
Elias
Maoni
Nia njema ya serikali kuweka na kufuata sheria na taratibu zinazosimamia biashara na masuala mengine ya jamii inaeleweka. Lakini baadhi ya hatua za utekelezaji zinapaswa kutazamwa kwa makini. Kwa mfano, mamlaka husika zinapovunja meza na vibanda vya kuuzia maandazi, chapati, samaki wa mafungu waliokaangwa, vilivyopo katika makazi ya watu wa kipato cha chini. Sidhani kama serikali imeandaa eneo maalumu la kuwakusanya wauza chapati, maandazi na samaki wa mafungu, wa jiji la Dar es Salaam. Wengi wa wauzaji hawa ni akina mama na binti zao. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba kwa biashara hizo wanalipa kodi za nyumba, kusomesha watoto na kutunza familia zao. Machinga wametengewa maeneo japo hayatoshi na hayana huduma muhimu. Lakini hawa akina mama wanapovunjiwa soko walilotengewa la chapati, maandazi na samaki wa mafungu liko wapi? Miradi ya TASAF haiwezi kuchukuliwa kuwa tayari imeleta neema kwa watu maskini. Si kweli. Na kama italeta neema, ni baadaye. Neema hiyo haijaonekana bado. Kuwavunjia akina mama hawa ni kuvunja tumaini lao pekee la kipato. Na si kwao tu bali wakazi wengi wa maeneo ya aina hii, mfano Tandika, Mwananyamala, Mbagala, Tabata, Buguruni na mengineyo, hutegemea sana kitoweo cha bei nafuu, wanachoweza kukimudu kutoka kwa wafanyabiashara hawa wadogo. Nia ya serikali ni njema, lakini sidhani kama kero kuu inayowapata Watanzania na kuwakosesha usingizi ni hizi meza na vibanda vya chapati, mchicha, samaki na viazi mbatambata(chips). Wanaumizwa zaidi na uporaji wa mabilioni ya fedha za nchi yao na ufisadi mkubwa uliochangia kuwafikisha baadhi yao katika hali hii ya kutegemea biashara za samaki wa mafungu, mchicha na maandazi. Walikwisha jeruhiwa vya kutosha kwa miaka mingi. Pale sheria zilipokuwa zikimilikiwa na wenye fedha. Na pale polisi na maafisa wa serikali walipogeuka kuwa majambazi au kushirikiana na majambazi. Wanateswa na mgao wa umeme ambao kwa kiasi kikubwa, licha ya tatizo la mvua, umesababishwa na ufisadi wa watawala wao. Watanzania wengi walio maskini walifikia mahali pa kukata tamaa na kupoteza matumaini. Kikwete alichangia kufufua mioyo yao. Sasa ningeiomba serikali isiwazidishie machungu hawa Watanzania walio maskini kwa kuwavunjia hata lile tegemeo lao la kipato, japo ni dogo na lisilo rasmi, lakini linawaokoa wao na watoto wao; hasa kwa yale maeneo ya makazi ya watu wa kipato ca chini.
